TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA
(TEWW)

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
UJUMBE WA SUDANI KUSINI WAVUTIWA NA KAZI ZA TAASISI YA ELIMU YA ELIMU YA WATU WAZIMA TANZANIA
UJUMBE WA SUDANI KUSINI WAVUTIWA NA KAZI ZA TAASISI YA ELIMU YA ELIMU YA WATU WAZIMA TANZANIA
28th Jul, 2025

UJUMBE WA SUDANI KUSINI WAVUTIWA NA KAZI ZA TAASISI YA ELIMU YA ELIMU YA WATU WAZIMA TANZANIA

‎Na Emmanuel Sanira, TEWW – Dar es Salaam

‎Kufuatia kuendelea kukua kwa sekta ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (EWW/ENMR) nchini, Tanzania imekuwa kivutio kwa nchi mbalimbali barani Afrika kuja kujifunza namna bora ya uendeshaji wa sekta hiyo.

‎Hayo yamethibitishwa kwa mara nyingine mwishoni mwa juma Julai 19, 2025 ambapo ujumbe wa viongozi waandamizi 11 kutoka Wizara ya Elimu na Ufundishaji nchini Sudani Kusini wakiambatana na Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Mh. Gloria Mambia ulipofanya ziara Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) na kujifunza masuala mbalimbali kuhusu uendeshaji wa Elimu ya Watu Wazima.

‎Katika ziara hiyo, Kiongozi wa ujumbe huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bwana Kachuol Piok amesema kuwa wamevutiwa sana na namna sekta ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ilivyopiga hatua kubwa nchini Tanzania.

‎Kiongozi huyo aliongeza kuwa yote waliyojifunza wataenda kuyatekeleza, na waliomba ushirikiano ulioanzishwa udumu ili nchi yake iendelee kupata uzoefu kutoka Tanzania.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa TEWW, Prof. Philipo Sanga amesema kuwa kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Tanzania), TEWW ipo tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika pindi watakapohitaji kujifunza zaidi na kubadilishana uzoefu ili kuinua maendeleo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini Sudani Kusini.

Pia, Prof.Sanga aligusia maeneo kadhaa ambayo TEWW inaweza kushirikiana na Sudani Kusini ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa walimu na kuimarisha program za elimumsingi nje ya mfumo rasmi.

‎Sambamba na hilo, Prof. Sanga aliukaribisha ujumbe huo kwenye Kongamano la Elimu Bila Ukomo lenye lengo la kuadhimisha miaka 50 ya TEWW tarehe 25-27 Agosti katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.