TEWW YATOA MSAADA WA VIAKISI KWA BODABODA MORO
Na Emmanuel Sanira - TEWW, Morogoro
Katika jitihada za kuelimisha umma kuhusu usalama barabarani jana (Julai 16, 2025) Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Kampasi ya Morogoro - WAMO imetoa mafunzo na msaada wa viakisi (reflectors) 20 kwa maafisa usafirishaji (bodaboda) wa mjini Morogoro.
Mafunzo na msaada huo vimetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake 1975, ambapo kilele chake kitakuwa Agosti 25 – 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Tembelea www.50years.iae.ac.tz kwa taarifa zaidi.
Akiongea katika hafla ya kukabidhi msaada huo mara baada ya mafunzo ya ulinzi na usalama barabarani, Kaimu Afisa Elimu Jamii (W) Morogoro, Insp. Kasimu Makadi ameipongeza TEWW kwa kuwaandalia maafisa usafirishaji hao mafunzo na kuwapatia vifaa muhimu kwa usalama wao na abiria wanaowabeba.
“... kupitia mafunzo haya, Taasisi itakuwa imetekeleza lengo lake, na jamii itaendelea kunufaika kupitia elimu hii; Hivyo, hongereni sana!” alisema Insp. Makadi.
Insp. Makadi aliongeza kuwa Jeshi la Polisi kupitia kikosi chake cha usalama barabarani litaendelea kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na TEWW ili kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi na kuwafikia maafisa usafirishaji wengi zaidi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Kampasi ya Morogoro – WAMO, Bwana Ferdinand Byenobi amesema kuwa TEWW inatambua umuhimu wa ulinzi na usalama kwa maafisa usafirishaji, hivyo katika maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi yake iliona vyema kuandaa mafunzo hayo na kutoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii inayowazunguka.
Kampasi ya TEWW Morogoro - WAMO ni miongoni mwa kampasi nne (4) za taasisi hiyo zinazotoa mafunzo ya ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada. Pia, Kampasi hizo zinatoa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi. Kampasi nyingine ni: Dar es Salaam, Mwanza na Ruvuma.