28th Jul, 2025
MKUU WA TEWW AMTEMBELEA BALOZI NICHOLAS KUHANGA
Na Emmanuel Sanira - TEWW
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga mwishoni mwa wiki (Julai 11, 2025) alimtembelea Mhe. Balozi Dkt. Nicholas Kuhanga nyumbani kwake Bunju, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumjulia hali na kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo elimu hapa nchini, hasa chimbuko la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Balozi Kuhanga (93) aliwahi kuwa Waziri wa Elimu mwaka 1978 kabla hajateuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – UDSM (1980 – 1988); na Balozi wa Tanzania katika nchi ya Kongo (1991 – 1992).
Wakati wa mazungumzo yao, Mhe. Balozi Kuhanga alimshukuru na kumpongeza Prof.
Sanga na ujumbe wake kwa kumtembelea na hasa kuendeleza juhudi za utoaji wa elimu ya watu wazima nchini.
Kiongozi huyo mwandamizi wa serikali mstaafu alimweleza Prof. Sanga na ujumbe wake
kuwa akiwa Waziri wa elimu alijitahidi kuinua elimu ya watu wazima nchini hadi aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere akampa nishani ya kutambua mchango wake katika sekta ya elimu ya watu wazima.
“Wakati ule, Hayati Mwalimu Nyerere akitoa hotuba ya kuhimiza elimu ya watu wazima nchini aliona vyema kunipa nishani ya kutambua kazi na mchango wangu wa kuinua elimu ya watu wazima hapa nchini, na nawapongeza sana kwa kazi mnayoifanya,” alisema Balozi Kuhanga.
Pia, Balozi Kuhanga aliupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu chini ya Prof. Adolf Mkenda kwa mageuzi makubwa katika mitaala ya elimumsingi nchini. Kuhusu mageuzi ya mitaala, Balozi Kuhanga aliishauri TEWW kuangalia namna ambavyo elimu ya watu wazima inapaswa iwe ili kuendana na mahitaji ya jamii ya sasa.
Kwa upande wake, Prof. Sanga alimshukuru Mhe. Balozi Kuhanga kwa mchango wake mkubwa kwa Taifa, na alisema utumishi wa Balozi Kuhanga kwa umma unayo mengi ya kujifunza ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa. Aliongeza kwa
kusema kuwa maarifa waliyoyapata kwake yatasaidia kuboresha utendaji kazi na kuinua
zaidi sekta ya elimu ya watu wazima na elimu nje mfumo rasmi nchini.
Kufanyika kwa ziara hii ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW yanayotarajiwa kufikia kilele chake Agosti 25 – 27 mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kwa Kongamano kubwa lenye kauli mbiu ya “Elimu bila ukomo, kwa maendeleo endelevu.”