IPOSA

Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio nje ya Shule (MECHAVI) (Integrated Program for Out of School Youths - IPOSA).

Mpango huu umeandaliwa na TEWW chini ya ufadhili wa UNICEF na unakusudia kutatua mahitaji ya kielimu miongoni mwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu nchini.MECHAVI inalenga makundi mahsusi ambayo ni pamoja na vijana ambao hawakuwahi kwenda shule, walioacha shule katika ngazi ya msingi na sekondari na waliomaliza darasa la saba lakini hawakuendelea na elimu ya sekondari. Mpango wa MECHAVI una maeneo makuu manne ya ujifunzaji. Maeneo hayo ni Stadi za KKK; Stadi za ufundi wa awali; Stadi za maisha na Ujasiriamali. Aidha uendeshaji wa MECHAVI unazingatia nadharia za unyumbufu na ujenzi wa umahiri katika ujifunzaji na ufundishaji.

Lengo Kuu la Programu

Lengo kuu la mpango huu ni Kuwa na vijana walioelimika, wenye maarifa, ujuzi na stadi za kuweza kuchangia kwa haraka katika maendeleo ya taifa na kuhimili ushindani.

Malengo Mahsusi ya IPOSA

Baada ya kuhitimu mafunzo walengwa wa IPOSA wataweza :-

  • Kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ili zimwezeshe kupata maarifa na ujuzi wa ufundi.
  • Kujitambua, kutambua haki zake, kuthamini na kukuza mahusiano, uzalendo, utu, maadili na uraia uliotukuka ili aweze kushiriki katika maendeleo.
  • Kumudu stadi za ufundi wa awalina
  • Kumudu stadi za elimu ya ujasiriamali itakayomwezesha kukabiliana na maisha yake na jamii inayomzunguka.

Mpangilio wa Programu ya IPOSA

  • Programu inatekelezwa katika hatua mbili:
  • Hatua ya kwanza kwa wasio na Stadi za Kisomo (KKK) na inachukua miezi mitatu hadi mitano
  • Hatua ya pili ni kwa wale walio na stadi za Kisomo ambayo huchukua miezi 12 hadi miezi 15.

Kwa sasa mpango unatekelezwa katika mikoa 8 ya Tanzania (Kigoma, Tabora, Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe) ambapo jumla ya vijana na watu wazima 10,000 wanatarajiwa kufikiwa.

  • Walengwa wakuu wa program ya IPOSA
  • I.Vijana ambao hawakuwahi kabisa kwenda shuleni kuanzia miaka 14 na kuendelea
  • II.Wanafunzi walioacha shule ya Msingi
  • III.Wanafunzi waliomaliza darasa la Saba na kukosa fursa ya kuendelea na masomo
  • IV.Wanafuni waliomaliza kupitia program ya MEMKWA.
  • V.Wasichana walioacha shule kwa changamoto mbalimbali kama vile ujauzito, ndoa za utotoni n.k

Fursa za IPOSA

Kupitia programu hii ya IPOSA kuna fursa mbalimbali zitakazopatikana zikijumuisha:

  1. Kumwezesha mwanafunzi mlengwa kupata elimu changamani kama sehemu mojawapo ya haki zake za msingi;
  2. Kuwa suluhisho muhimu kwa makundi mbalimbali ya watu wazima na vijana, walioshindwa kupata elimu hiyo, kwa sababu mbalimbali kuona kwamba ndoto zao sasa zinaweza kufikika pasipo kuwepo kikwazo chochote;
  3. Kuwepo kwa wadau mbalimbali ambao wanaweza kubuni, kuanzisha, kufadhili na kuendeleza utekelezaji wa programu hii;
  4. Kuwa na wigo mpana wa uendelezaji wa sayansi na teknolojia, ICT, utandawazi na ushirikiano wa kikanda kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo yao kiuchumi na kuimarisha ustawi wa jamii zao;
  5. Kuwepo kwa vitendea kazi (ambavyo vimeshanunuliwa na kupelekwa mikoani), majengo na miundombinu rafiki kwa kundi lengwa la wanafunzi; na
  6. Kuwepo kwa muitikio chanya na baraka za serikali yetu ya Jamhuru ya Muungano wa Tanzania kuhusu uendeshaji na uendelezwaji wa mpango hii.

Sababu za Progamu

IPOSA inakusudia kutatua changamoto mbalimbali kwa vijana lengwa kama zifuatazo:-

  • Kuwa njia mbadala ya kupunguza kasi ya ongezeko la mahitaji ya elimu na ufundi kwa walengwa walio nje ya shule
  • Kuunga mkono harakati za serikali katika kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
  • Kuandaa vijana watakaoshiriki kikamilifu kutekeleza kwa vitendo sera ya viwanda
  • Kuongeza fursa za elimu na mafunzo ya ufundi kwa vijana wa kundi rika la 14-17; hususan walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ya sekondari.
  • Kuongeza wigo wa elimu sawia / linganifu (equity) ya kujiendeleza kwa vijana katika mazingira anuai.
  • Kuongeza wigo kwa vijana kupata ujuzi na maarifa ya kuweza kuchangia maendeleo binafsi na ya Taifa kwa ujumla.

Muktadha wa Programu

IPOSA imeandaliwa katika muktadha wa msisitizo wa Elimu kwa Wote, na uboreshaji wa upatikanaji wa elimu kwa watoto na vijana walioikosa. Msisitizo wa Elimu kwa Wote umeongeza idadi ya vijana wanaojiunga na IPOSA. Maendeleo ya sayansi na teknolojia, utandawazi, sera ya viwanda na dira ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati; inachagiza vijana wawezeshwe kukabiliana na mabadiliko endelevu kwa kuzingatia usawa wa mahitaji kulingana na mazingira na rasilimali zinazowazunguka.

Matarajio ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

  1. Kuwezesha vijana na watu wazima pamoja na makundi mengine ndani ya jamii kupata elimu, stadi za kazi, ujuzi na maarifa ili zitumike kama chachu na nyenzo muhimu kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha;
  2. Kuwezesha taifa kutokuwa na wananchi wasiokuwa na ujuzi, stadi nyenzo na maarifa ya kutosha ili taifa liwe na nguvu kazi stahiki kwa maendeleo ya jamii;
  3. Kuondokana na jamii ya watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kama msingi muhimu wa elimu;
  4. Kuwezesha kila raia kuwa na uwezo, fursa na shauku ya kushiriki moja kwa moja katika harakati za uanzishwaji wa miradi ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii katika nchi yetu.